Thursday, October 4, 2012

Mtafaruku wazuka makaburini Bagamoyo


Mtafaruku umezuka Wilaya ya Bagamoyo baada ya watu wanaodhaniwa kuwa waumini wa dini ya Kiislamu wa msikiti wa Majani Mapana kuvamia makaburi ya kiislamu ya Tandika Kata ya Magomeni kwa lengo la kutaka kubomoa kaburi moja la mtoto Aruina Rolan Mitaban.

Watu hao walitaka kubomoa kaburi hilo wakidai kuwa mtoto aliyezikwa katika makaburi hayo  ni Mkristo, hivyo haruhusiwi kwa kuwa si muumini wa dini ya Kiislamu.

Tukio hilo limetokea juzi wa Jumapili na waumini hao baada ya kulibomoa kaburi hilo, waliwataka ndugu wa marehemu kufukua mwili wa mtoto huyo kabla wao hawajachukua hatua za kufukua.

Walisema kitendo cha Wakristo kwenda kuuzika mwili huo katika makaburi hayo na kuujengea kwa marumaru na kuweka msalaba ni uchokozi kwa waumini wa dini ya Kiislamu.

Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, alilazimika kuitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Ulinzi na Usalama suala hilo ili kulipatia ufumbuzi.

Kipozi aliwataka waumini wa dini zote mbili kujenga tabia ya kuvumiliana wanapokuwa na matatizo badala ya kuendekeza jazba na hasira ambazo haziwezi kuleta tija.

Mwili wa mtoto huo baada ya kufukuliwa na ndugu wa marehemu walikwenda  kuuzika upya jijini Dar es salaam.

Aidha, alisisitiza kuwa  viongozi wa dini hizo wahakikishe  wanasiliana na ofisi yake ili kushughulikia matatizo kama hayo mara moja yanapotokea.

“Nawapongeza ndugu wa marehemu kwa watulivu na kuamua kufukua kaburi la ndugu yao bila kuleta pingamizi, hawa wameonyesha uzalendo wao wakuitakia nchi yetu amani iliyopo isitoweke,” alisema.

Baadhi ya ndugu wa marehemu huyo walisema kitendo kilichofanywa na waumini hao si kiungwana kwani kama kulikuwa na tatizo iliwapasa kwenda kuwataarifu badala ya kusambaratisha kaburi hilo. 

No comments: