Wednesday, November 14, 2012

Sizitaki Mbichi hizi - Hii ni kwa wale wa zamani

Hadithi inayokuja, ni ya Sungura sikia,
Hadithi uliyongoja, leo ninakuletea,
Alitoka siku moja, njaa aliposikia,
Njaa aliposikia, Sungura nakuambia

Siku ile akaenda, Porini kutembelea,
Akayaona matunda, mtini yameenea,
Sungura akayapenda, mtini akasogea,
Mtini akasogea, Sungura nakuambia.

Sungura karukaruka, lakini hakufikia,
Matunda hakuyashika, mikononi hakutia,
Hakika alisumbuka, nguvuze zikapungua,
Nguvuze zikapungua Sungura nakuambia.

Mtazame hapo juu Sungura amelegea,
Mtazame na miguu, matunda anarukia,
Atafanya sikukuu, matunda akifikia,
Matunda akifikia, Sungura nakuambia.

Karuka tena karuka, matunda akarukia,
Mwisho wake akachoka, kachoka hata mkia,
Penye mti akatoka, pembeni akasogea,
Pembeni akasogea, Sungura nakuambia.

“Sizitaki mbichi hizi” Sungura akagumia,
“Naona nafanya kazi, bila faida kujua”,
Yakamtoka machozi matunda akalilia,
Matunda akalilia, Sungura nakuambia.

Sio kama hakutaka, sasa nakupasulia,
Matunda aliyataka, ndiyo kisa akalia
Tunajua hakufika, alichoka kurukia,
Alichoka kurukia, Sungura nakuambia.

Hadithi nimemaliza, nimekwisha simulia,
Jambo moja sikiliza, rafiki yangu sikta,
Usikose kujikaza, mazuri kukazania,
Utamshinda Sungura, utapata mbivu hizi

No comments: