Thursday, July 5, 2012

KUANZISHWA KWA CHAMA CHA WANYWAJI POMBE TANZANIA



Leon Bahati
KILA mwaka Serikali imekuwa ikiongeza kodi kwenye vinywaji, hususan pombe ili kukidhi  bajeti ya mapato na matumizi yake. Hali hiyo husababisha bei ya pombe kupanda karibu kila mwaka na kuwaongezea mzigo wanywaji kwa kulazimika kuzama zaidi kwenye mifuko yao ili kugharimia kinywaji hicho.Kwa miaka yote hiyo wanywaji wamekuwa wakilia kimoyomoyo bila ya  kuwa na mahali pa kupaza sauti zao, hali inayoifanya Serikali ione kinywaji ni mahali kukimbilia kupata fedha.

Kulingana na taarifa za viwanda vya bia, bei ya kinywaji hicho huenda ikapanda kwa karibu asilimia 25, kuanzia mwezi huu, jambo ambalo limewafanya wanywaji kusema; “Hapana! Haiwezekani.”
Kwa sababu hiyo, wanywaji tayari wameunda jukwaa lao la kupaza sauti zao na tayari wameweka mikakakati ya kudai haki zao.Chombo hicho wamekipa jina “Chama cha Wanywa Pombe kwa Staha Tanzania (TRBDA)” na tayari kimesajiliwa na sasa kipo katika harakati za mikakati ya kukabiliana na Serikali.

“Sisi tunachotaka ni bei ya bia kushuka au kubakia palepale (Sh1,700). Hili ni suala nyeti na hatari kuliko watu wanavyolifikiria sasa,” anasema Rais wa TRBDA, Gasisi Mahuti.
Anaongeza; “Chama kimesajiliwa Mei 22 mwaka huu, hivyo tuna nguvu ya kisheria kufanya kazi na kutetea maslahi ya wanachama wetu.
“Tunaona kero kila mwaka, kila Bajeti ya Serikali wanakuja na mikakati ya kuongeza kodi kwenye pombe.”
Mahuti anasema kwa miaka mingi mzigo huo wa ongezoko la bei ya bia ambayo ndiyo inayotumiwa na watu wengi, imekuwa ikiongezeka, lakini safari hii, hali ni mbaya zaidi.
Mzigo huo kwa wanywaji anasema umechangiwa na mambo mawili makubwa ambayo ni kuongezeka kwa gharama za maisha na kiwango kikubwa cha kodi kwa mwaka huu wa fedha 2012/13 ulioanza leo.
“Hiyo bei itasababisha wanywaji wengi kuhama kwenye kinywaji salama na kwenda kwenye kinywaji hatarishi na haramu,” analalamika Mahuti.

SOURCE: http://mwananchi.co.tz

No comments: