Friday, August 24, 2012

Hekaya za Abunuwas - Juha haliambiliki!Juha haliambiliki!


SAFARI moja Juha alikaa mwisho wa tawi la mti, akilikata tawi hilo kwa kutumia msumeno. Akapita mtu mmoja akamtahadharisha kuwa kitendo alichokuwa akikifanya ni cha hatari. Alimwambia kuwa lile tawi likikatika naye ataanguka! Alimshauri akae kwenye shina la tawi atanusurika.

Juha hakutaka kabisa kusikiliza ule ushauri aliopewa. Alimgeukia yule mtu na kumwambia, "Wewe imekuhusu nini? Nikianguka, mimi ndiye nitakayeumia! Hebu achana na mimi, shika njia uende zako!"

Yule mtu, ingawa alikuwa ana hakika kuwa Juha ataanguka tu, lakini hakuwa na njia ya kumzuia. Akaona bora aende zake. Juha alipomwona anaondoka akaaanza kumpigia kelele, "Mtanzameni huyo. Hana analolijua isipokuwa kuwaombea wenziwe mabaya tu".

Yule bwana akajifanya kama hakuwa akiyasikia yale aliyokuwa akiambiwa. Lakini alikuwa akisema moyoni, "Asiyesikia la mkuu, huvunjika guu!" Kabla hajafika mbali akasikia kishindo na mayowe yakipigwa. Alipogeuka akamwona Juha yuko chini na lile tawi la mti lamwelemea juu yake. Anapiga kelele kuomba msaada. Basi yule mtu akawaita wapita njia, wasaidiane kumwokoa Juha. Walifanikiwa kumnusuru, lakini Juha alikuwa ameumia kiuno!

Yule mtu akamwuliza Juha, "unalia nini? Ungelisikiliza maneno yangu yangalikufika haya?" Juha akajibu, "kweli ningalikusikiliza uliyoniambia nisingalianguka! Lakini mimi sikuwa nikijua kuwa wewe una ujuzi wa kutabiri mambo yajayo, ndiyo maana niliudharau ushauri wako. Kwa vile sasa nimeelewa kuwa wewe ni bingwa wa kutabiri basi niambiye na siku yangu ya kufa!" Yule mtu akastaajabu sana kwa swali hilo. Akamwuliza Juha, "Tokea lini mtu akaweza kuagua siku ya kifo cha mtu mwengine?" Juha akamjibu, "Mbona ulitabiri kuwa ningeanguka, na kweli nikaanguka? Basi hapana shaka, na siku yangu ya kufa unaijua!"

Yule mtu ilipombainikia kuwa yule hakuwa Juha wa jina tu, bali hata wa vitendo, aliamua kumwacha kama alivyo, na kuendelea na safari yake.

Kisa hiki si cha kweli. Ni katika zile hekaya za Abunuwasi. Ni hadithi za PAUKWA, PAKAWA! Lakini ni kisa chenye mazingatio makubwa kwa yule mwenye kutaka kuzingatia. 

Je wewe msomaji unajifunza nini juu ya kisa hiki?

No comments: