
Imeonekana kuwa hatua isiyokuwa ya kawaida.
Wizara ya ulinzi ya
Afrika Kusini imethibitisha kuwa kambi zote za kijeshi zimewekwa katika hali ya
tahadhari kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1994. Yote haya ni kutokana na mpango
wa Julius Malema kutaka kuzungumza na baadhi ya wanajeshi.
Bwana Malema ni
mwanasiasa anayeibua mgawanyiko hapa. Hivi maajuzi alifukuzwa kutoka chama cha
ANC na kwa sasa anafanyiwa uchunguzi kuhusiana na kashfa ya ufisadi.
Lakini hajaondoka ANC
kimya kimya. Badala yake ametumia mauaji ya hivi maajuzi katika mgodi wa
marikana kuanzisha kampeni kali dhidi ya mabepari nchini Afrika Kusini na
kutaka yafanyike mapinduzi ya kiuchumi. Wengi wanamshutumu kwa kuhusika na
ubinafsi mbaya wa kisiasa, lakini Malema anapokea uungwaji mkubwa kutoka kwa
jamii za watu maskini na kimya cha serikali ni ishara tosha kuwa imeshindwa
kukabiliana naye.
Manung'uniko ya
wanajeshi ni fursa nyingine kwa Malema kuonyesha ubabe wake na hali ni tete
nchini Afrika Kusini. Hofu iliyopo ni kwamba migomo huenda ikaenea zaidi na
kwamba serikali kwa sasa inazingirwa na migogoro ya ndani huku baadhi ya
mirengo serikalini ikipanga njama ya kumtimua madarakani Rais Jacob Zuma.
Source:
BBC Swahili.
No comments:
Post a Comment