
Afisa mmoja wa ubalozi wa Marekani ameuawa na wengine wamejeruhiwa wakati kundi la watu waliojihami na silaha walipovamia jengo hilo mjini Benghazi.
Maandamano pia
yamefanyika mjini Cairo, Misri. Inaaminika kuwa watu
hao walikuwa wanaandamana kulaani filamu mmoja iliyotengenezwa nchini Marekani
ambayo wanasema inamkejeli Mtume Mohammed.
Jengo hilo
liliteketezwa kabisa na wandamanaji hao waliokuwa na hasira. Maandamano hayo
yalichochea makabiliano kati ya vikosi vya serikali na kundi la wanamgambo
maarufu kama Ansar al Sharia brigade, mjini Benghazi.
Msemaji wa serikali ya
Marekani, amelaani kitendo hicho na ameongeza kuwa wanashirikiana na idara ya
usalama nchini Libya kuimarisha usalama kwenye balozi zake. Taarifa zinasema
kuwa wakaazi wa mji mkuu Tripoli, wamekuwa wakishawishiwa kupitia ujumbe kwenye
tovuti za kijamii wafanye maandamano lakini hakuna aliyejitokeza.
Sehemu ya filamu hiyo
inasambazwa kupitia mtandao wa Youtube kwa lugha ya kiarabu. Maandamano sawa na
hayo pia yamefanyika mjini Cairo nchini Misri. Kundi lingine la watu limeingia
kwenye ubalozi wa Marekani na kuteketeza bendera ya nchi hiyo. Taarifa kutoka
Cairo zinasema, maelfu ya Waislamu na Wakristo wameungana kulaani filamu hiyo.
Hata hivyo hakuna aliyejeruhiwa kwenye maandamano hayo yaliyofanyika nchini Misri.
Source: BBCswahili
No comments:
Post a Comment