![]() |
Kero la wananchi wa Kenya kwa wabunge wao |
Wabunge hao walipanga kujilipa dola elfu mia moja na kumi kila
mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Lakini Rais Kibaki amesema kuwa hatua hiyo
inakiuka katiba na haiwezi kutekelezwa wakati ambapo walimu pamoja na madaktari
nchini Kenya wamekuwa wakigoma kudai nyongeza ya mishahara. Waandamanaji
waliojawa na ghadhabu nchini Kenya walijitokeza hapo jana kulaani hatua ya
wabunge hao kutaka kujilipa mamilioni ya pesa kama pesa za ziada wakati bunge
litakapofunga vikao vyake kwa maandalizi ya uchaguzi mwaka ujao. Waliwataja
wabunge hao kama fisi wenye ulafi.
Wabunge wa Kenya ni baadhi ya wale wanaopokea mishahara mikubwa
sana barani Afrika , wakipokea takriban dola elfu 10,000 kama mshahara kila
mwezi. Malipo hayo ya ziada ya dola 110,000 kwa kila mmoja walitaka yalipwe
wakati watakapofunga vikao vyao kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka 2013.
Wadadisi wanasema kuwa wananchi wangetozwa kodi zaidi ili
kugharamia malipo hayo ya dola milioni 23. Hatua hii imewakasirisha watu wengi,
hasa ikizingatiwa kuwa inakuja baada tu ya migomo katika sekta ya umma ambapo
madaktari, walimu na hata wahadhiri wa vyuo vikuu walisusia kazi wakidai
nyongeza ya mishahara. Mswaada huo ulipitishwa siku ya Alhamisi ikiwa sehemu ya
mabadiliko yaliyofanyiwa mswaada wa fedha bungeni.
Mnamo mwezi Septemba, shule za umma zilifungwa kwa wiki tatu
wakati walimu walipogoma wakidai nyongeza ya mishahara na huku madaktari nao
wakitaka mazingira bora ya kazi.
No comments:
Post a Comment