Sunday, July 29, 2012

Wabunge mafisadi watajwa - SPIKA AVUNJA KAMATI YA NISHATI, WAZIRI AELEZA WALIVYOITAFUNA TANESCO


WAKATI wabunge wakitoa tuhuma nzito dhidi ya wenzao wanaodaiwa kujihusisha na ufisadi ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), imebainishwa kuwa wabunge wenye tabia hiyo ni watano, watatu kutoka chama tawala CCM na wawili upinzani.

Habari zilizopatikana jana mjini Dodoma zimeeleza kuwa baadhi ya wabunge hao wanatoka katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, huku wengine wakitoka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma. 

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wabunge hao wamedaiwa kuwa wamekuwa wakitumia nafasi zao za ubunge na ujumbe wa kamati kufanya biashara na Tanesco na kutetea mafisadi ndani ya shirika hilo la umma.

Gazeti hili limefanikiwa kupata majina ya wabunge hao, ambayo leo hatutayataja kwa sababu za kitaaluma. 

Baadhi ya wabunge waliochangia hoja hiyo bungeni juzi na jana walisema kuwa, wanawafahamu wabunge hao kwa majina, lakini hawapendi kuwataja kwa kuwa siyo wakati mwafaka.

Moto wa kutaka kutajwa kwa majina ya wabunge hao ulikolezwa jana na Mbunge Vita Kawawa wa Namtumbo(CCM) aliyeomba Mwongozo wa Spika, akitaka jambo hili lijadiliwe na Bunge na kupendekeza kuwa, Kamati za Bunge zinazotuhumiwa kwa rushwa zivunjwe.

 “Waheshimiwa wabunge wamejadili suala hili kwenye wizara, lakini kwa mujibu wa kifungu cha 55 (3)f  mbunge au waziri anaweza kutoa hoja ili jambo fulani lijadiliwe. Sasa naomba kutoa hoja ya kujadili suala hilo," Kawawa alisema.

Aliliomba pia Bunge likubali kuivunja na kuiunda upya Kamati ya Nishati na Madini na kamati nyingine zilizolalamikiwa kwa rushwa. Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge. 

Baada ya hoja hiyo kuungwa mkono Spika wa Bunge, Anne Makinda alisimama na kukubali hoja hiyo ya Kawawa na kutangaza kuivunja Kamati ya Nishati na Madini.

Spika Makinda alisema ameiagiza Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kutengeneza kanuni za kuwadhibiti wabunge wenye tabia hiyo ya kupokea rushwa kutoka kwa watu mbalimbali ili kutimiza matakwa yao binafsi.

"Ninakubali kuivunja Kamati ya Nishati na Madini na zingine ambazo zitatajwa kwenye tuhuma hizo. Nalipeleka pia suala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, halafu kama ni kutajwa (wabunge hao), basi tutapata mwongozo wa kamati hiyo." alisema Spika Makinda na kuongeza:

"Nasema kwa dhati kabisa, kitendo hiki hakikubaliki ndani ya Bunge hili. Wabunge mkae vizuri. Kama kuna baadhi yetu wanaenda huku na huku kujitafutia masilahi binafsi, tutawezaje kuisimamia Serikali?"

SOURCE: Gazeti la Mwananchi.       KUSOMA ZAIDI GONGA HAPA:  Wabunge mafisadi wa Tanesco


No comments: