Friday, August 24, 2012

Khanga yazua sokomoko.. Mambo ya pwani hayo..



Mpenzi na mshabiki wetu wa Lamu ametupeperushia majina ya khanga mpya zilizotoka karibuni huko Mombasa. Kwa hakika tunamshukuru sana dada huyu kwa moyo wake wa kujituma ili kutufungua macho na kutupa burudani tulioko ughaibuni. Kwa anaependa kuagiza khanga hizi atuandikie barua pepe kwa maelekezo ya kuzipata:-

1. Raha ya dodo lisiwe dogo
2. Uzuri wa shavu liwe kavu
3. Baniani mbaya kiatu chake dawa kwa asie haya..
4. Kuku hujamjulia bata utamuweza?
5. Mpenda ngulu haogopi shombo
6. Hupati hata kwa dawa
7. Penye mzoga hapakosi inzi
8. Hata kwa dawa humpati
9. Hima hima nikupe anachokunyima
10. Wenzio twaoga wewe waroga

11. Panda juu kwa Mungu ukazibe

12. Sherehe si yako jamvi la nini?
13. Muonja asali haonji mara moja
14. Mla nawe hafi nawe ila mzaliwa nawe
15. Mpakua choo haogopi mavi
16. Kama mali panda mahindi
17. Ya juzi lakini huitunzi
18. Kama mboga wee bamia
19. Radhi ni bora kuliko mali
20 Akumulikae mchana usiku atakuchoma  


Pamoja na kunitumia orodha ya kanga hizo shabiki wetu wa Lamu amenifahamisha kwamba bwana mmoja mkazi wa Lamu amempa talaka tatu mkewe baada ya kutoridhika na maneno yaliyokuwa yameandikwa katika Khanga aliyokuwa amevaa mkewe. Bwana huyo ambae alikuwa safarini kwa muda wa miezi miwili alishituka aliporudi nyumbani na kumkuta mkewe akiwa amevaa kanga mpya iliyoandikwa "Kuliko kioze heri nimpe jirani". Mume huyo mwenye wivu alimjia juu mkewe na kudai aelezwe mkewe alikuwa ana maana gani kuvaa kanga hiyo wakati yeye akiwa safarini. Wakati mwanamke akijaribu kujitetea, mwanaume akaiona khanga nyingine mpya iliyoelekea kuvaliwa mara kadhaa ambayo ujumbe wake ndio uliomfanya atoe talaka. Khanga hiyo ilikuwa imeandikwa "Nitoe hamu, nipe utamu mpaka anywe sumu..."

No comments: