UTAJIRI wa kutisha baadhi ya viongozi wa dini nchini umezua mjadala mzito katika jamii, huku baadhi ya watu wakisema hautokani na neema ya Mungu. Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa baadhi ya viongozi hao wa dini hasa wa madhehebu ya Kikristo, wengi wanaoongoza makanisa yao, sasa wana utajiri mkubwa wenye thamani ya mabilioni ya fedha. Baadhi ya mali zinazomilikiwa na viongozi hao wa dini ni pamoja na majengo makubwa, yaliyo na thamani ya mabilioni ya fedha, vyombo vya habari, taasisi za fedha, magari ya kifahari na miradi mingine inayowaingizia mamilioni kila siku. Hata hivyo, viongozi wanaotajwa kuwa na utajiri wamepinga hoja hiyo wakisema kuwa utajiri walionao ni neema ya Mungu.
Askofu Isangya
Askofu Mkuu wa Kanisa la International Evangalism Church (IEC) lenye makao makuu yake eneo la Sakila wilayani Arumeru mkoani Arusha, Eliud Isangya alisema ya kuwa haoni tatizo kwa viongozi wa dini nchini kumiliki mali ikiwamo magari ya kifahari, nyumba na fedha, akieleza kuwa hizo ni baraka kutoka kwa Mungu. Hata hivyo, Isangya alisema kuwa mbali na kumiliki mali hizo, jambo la muhimu kwa viongozi hao ni kufuata katiba za makanisa yao na kwamba, huenda mali hizo zikatokana na mishahara ya kazi zao.
“Sioni kikwazo chochote kwa viongozi wa dini kuwa na mali kwa kuwa hiyo ni baraka kutoka kwa Mungu, lakini iwe kwa mujibu wa katiba za makanisa yao,” alisema Isangya.
Askofu huyo anayedaiwa kumiliki ndege na uwanja wa ndege karibu na kanisa lake eneo la Sakila mjini Arusha, alisisitiza kwa kutoa mifano kuwa Mungu aliwabariki Nabii Suleiman na Abraham wakawa na mali nyingi zikiwamo dhahabu kutokana na kazi zao. Alisisitzia kuwa kigezo cha mtumishi wa Mungu kuwa maskini siyo msingi wa Biblia na kuwa, waumini wake hawana tatizo lolote naye. Hata hivyo hivyo alisema kuwa, yeye hapendi kuwa na mali kupindukia, bali ametanguliza huduma ya Mungu pamoja na kulea yatima.
Mchungaji Gwajima
Msemaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mchungaji Yekonia Bihagaza lililopo eneo la Kawe Kiwanda cha Tanganyika Parkers, ambaye ni msaidizi wa kiongozi wa kanisa hilo Mchungaji Josephat Gwajima, alisema kuwa magari wanayotembelea wachungaji wa kanisa hilo yanatokana na misaada inayotolewa na waumini wao. Bihagaza alisema kuwa jamii imekuwa na mtazamo tofauti kuhusu mali zinazomilikiwa na wachungaji, jambo alilosema linashangaza.
“Gari analotumia mtumishi (Gwajima) ni zawadi ya kihuduma, baada ya kutembelea nchi za nje katika kueneza Injili. Hata magari ya wachungaji wengine waliopo hapa ni zawadi tu. Kanisa hili linajiendesha lenyewe pasipokuwa na miradi mingine,”alisema Bihagaza.
Alisema kuwa mchungaji kuwa na mali au utajiri siyo jambo baya wala dhambi na kuongeza kuwa, kama atakuwa na miradi inayoingiza fedha nje ya kanisa, atakuwa na nafasi ya kumiliki gari lolote analopenda kutumia. Akitaja mali za kanisa hilo Mchungaji Bihagaza alisema kuwa kanisa hilo halina umiliki wa mali nyingi mbali na mabasi ya kusafiria mikoani kwa ajili ya kusambaza huduma.
“Akaunti yenyewe kwa sasa haiwezi kuwa na zaidi ya Sh2 milioni, hatuna mradi wa aina yoyote ile ambao unaingiza pesa. Pesa ya sadaka inayopatikana hapa kila Jumapili hutumika kuendesha shughuli za hapa kanisani,”alisema. Alikiri kuwapo kwa baadhi ya madhehebu ya kilokole, yanayotumia makanisa kama sehemu ya biashara na kusisitiza kuwa, hali hiyo ni kinyume na agizo la Mungu.
Naye Mchungaji Isaya Sizya wa Kanisa la Blessing Alter lililopo jijini Arusha, alisema kwamba kitendo cha baadhi ya viongozi wa dini kumiliki mali huku waumini wao wakiteseka katika lindi la umaskini hakikubaliki mbele ya Mungu na ni aibu kwa viongozi hao. Kuhusu yeye binafsi alisema kuwa mbali ya kuwapatia Waumini wake Neno la Mungu, pia amekuwa akiwasaidia kwa kuwainua kiuchumi ikiwamo kuwataka waanzishe vikundi vya kusaidiana.
Katibu Pentekoste anena
Katibu wa Makanisa ya Pentekoste, David Mwansota alisema kuwa, miaka ya hivi karibuni kumekuwa na wachungaji wanaoanzisha makanisa bila kuijua vizuri Biblia Takatifu wala sheria za kuanzisha makanisa.
“Wananchi wanatakiwa kuwa waangalifu sana na wachungaji wa aina hii kwa sababu, wengi hawafahamu sheria na kufuata Katiba ya kuongoza huduma zao,” alisema Mwansota.
Alifafanua kwamba kimsingi kanisa linapaswa kuwa na Katibu, Bodi, Mweka Hazina na vikao mbalimbali vya bodi. “Serikali inatakiwa kuliangalia suala hili kwa kina, kwani watu wanaweza kuzungumzia habari kuhusu kanisa fulani, wakaishia kuelezwa kuwa wanaona wivu na huduma husika,” alisema Mwansota.
Kanisa linapoendeshwa bila kufuatwa kwa sheria wala Katiba linaweza kukumbwa na migogoro kwa sababu hakuna wa kumhoji pale mambo yanapokwenda kombo. alisema Mwansota. “Utajiri wa mchungaji wa kanisa fulani unaweza kuwa halali au haramu. Unajua kuna makanisa mengine mshahara wa mchungaji unatokana na fungu la kumi wanalotoa waumini, pia yapo ambayo mshahara wa mchungaji unapangwa na bodi,”
Askofu Kilaini
Askofu Msaidizi Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini alisema kuwa hatua ya baadhi ya viongozi wa dini kutumia nafasi hiyo kujipatia mali siyo jambo zuri. Kilaini alisema kuwa kiongozi wa dini anatakiwa kuwatumikia waumini kwa kila kitu na siyo kutumia kigezo hicho kujipatia mali na utajiri mwingine. Aliitaka Serikali kudhibiti na kufanya ukaguzi wa usajili wa taasisi hizo za dini, akieleza kuwa baadhi ya viongozi wanatumia mwanya huo kuingiza mali na kujimilikisha binafsi.
Askofu Ngoyani
Wakizungumza kwa nyakati tofauti , Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Lindi, Mhashamu Bruno Ngonyani na Canon Douglas Msigala, wa Kanisa la Anglikana la Lindi walisema kuwa umefika wakati sasa wa Serikali kuzifuatilia taasisi za dini, ambazo viongozi wake wanatumia nafasi zao kujinufaisha. Askofu Ngonyani alisema kuwa viongozi wa dini ni wasimamizi na watunzaji wa mali za kanisa kwa manufaa ya waumini wao, hivyo ikitokea kiongozi binafsi anahodhi na kutumia mali hizo kwa manufaa binafsi hana tofauti na fisadi.
Mkoani Mbeya, baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini wameitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kufuatilia akaunti za wachungaji wanaomiliki mali nyingi ili kubaini vyanzo vyao halisi vya mapato hayo.
Maaskofu Nigeria
Wakati mjadala wa utajiri wa viongozi wa dini nchini ukiendelea kupamba moto, nchini Nigeria, maaskofu watano wanaomiliki makanisa yao, wametajwa na Jarida la Kimataifa la Forbes kuwa ndio wanaoongoza kwa utajiri. Viongozi hao wanaelezwa kumiliki miradi mikubwa ya mabilioni ya fedha, majengo, ndege na magari ya kifahari ikiwamo Daimlers, Porsches, BMW, don Rolexes na Patek Phillipes.
Anayeongoza kwa utajiri miongoni mwa viongozi hao wa kanisa nchini humo ni Askofu David Oyedepo akimiliki Kanisa la Living Faith World Outreach Ministry, maarufu kama Winners Chapel ambapo utajiri wake unakadiriwa kufikia Dola 150 milioni za Marekani sawa na Sh240 bilioni. Oyedepo aliyeanzisha kanisa hilo mwaka 1981 ni mmoja wa viongozi wa dini nchini Nigeria mwenye waumini wengi akimiliki kanisa lenye uwezo wa kuchukua watu 50,000, ndege nne kubwa zilizopo katika matawi yake Nigeria, Uingereza na Marekani pamoja na kampuni ya uchapaji, Chuo Kikuu na shule nyingi za sekondari.
Askofu Chris Oyakhilome
Askofu Chris Oyakhilome mwenye kanisa lililo na matawi jijini London, Afrika Kusini, Canada na Marekani anamiliki kampuni za uchapaji, vituo vya televisheni, magazeti, majarida, hoteli za kitalii , utajiri wake unakisiwa kufikia Dola za Marekani 30 milioni hadi 50 milioni.
Askofu Temitope Joshua
Askofu Temitope Joshua maarufu kama TB Joshua ana utajiri unaokadiriwa kufikia Dola za Marekani 10 milioni hadi 15 milioni akiwa mwanzilishi wa Kanisa la Synagogue Church of Nations.
Askofu Matthew Ashimolowo
Utajiri wake unafikia Dola 6 milioni za Marekani hadi 10 milioni, anashika namba ya nne kwa utajiri miongoni mwa viongozi wa dini nchini Nigeria. Ni mwanzilishi wa Kanisa la Kingsway International Christian Centre (KICC) huku mshahara wake kwa mwaka ukiwa ni zaidi ya Dola 100,000 za Marekani.
Chris Okotie
Askofu Chris Okotie anashika nafasi ya tano kati ya viongozi wa dini wanaoongoza kwa utajiri nchini Nigeria akiwa na utajiri wa Dola 3 milioni hadi 10 za Marekani. Alianza kama mwanamuziki wa kawaida kabla ya kuanzisha kanisa lake. Amewahi kugombea urais wa nchi hyo katika uchaguzi wa mwaka 2003, 2007 na mwaka 2011.
SOURCE: http://www.mwananchi.co.tz/news
|
Monday, September 24, 2012
Utajiri wa viongozi wa dini unatisha............HII SASA NI BALAA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment