![]() |
Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Omran Ben Shaaban |
Zaidi ya watu 10,000 nchini Libya walikusanyika kuomboleza kifo cha mmoja wa waasi waliosifika kwa kumkamata hayati Muammar Gaddafi mwaka jana. Omran Ben Shaaban alifariki Jumanne iliyopita baada ya kutekwa , kupigwa risasi na kuteswa na wafuasi wa hayati Gaddafi.
Mwili wa kijana huyo
aliyekuwa na umri wa miaka 22, ulipelekwa nyumbani kwao mjini Misrata kwa
mazishi. Serikali ilisema kuwa itampa mazishi ya kishujaa kijana huyo huku
kukiwa na wito wa serikali kulipiza mauaji yake. Omran Ben Shaaban alikamatwa na watu
waliokuwa wamejihami mnamo mwezi Julai, na kuzuiliwa kwa siku 50 mjini Bani
Walid, ilipokuwa ngome ya Gaddafi Kusini Mashariki mwa Tripoli. Aliachiliwa
wiki jana baada ya juhudi za upatanishi kufanywa na kiongozi wa mpito wa nchi
hiyo Mohammed Magarief.
Bwana Omran Ben Shaaban
aliwasili mjini Misrata akiwa na alama za mateso pamoja na alama ya risasi
kwenye uti wake wa mgongo. Alipelekwa mjini, Paris kwa matibabu ingawa
alifariki baadaye. Omran Ben Shaaban alianza kujulikana tarehe 20 mwezi Oktoba mwaka jana,
wakati alipoonekana katika sehemu alikokamatwa marehemu Kanali Gaddafi mjini
Sirte. Wengi wameomboleza kifo chake, aliyetambulika kama shujaa huku
serikali ikisema itafanya juhudi za kuwasaka watesi wake na kuwahukumu.
No comments:
Post a Comment